Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Hawza, kikao cha kila wiki cha darsa ya maadili cha Ayatullah Jawadi Amuli kilifanyika leo Jumatano, tarehe 13 Aban 1405 (4 Novemba 2026), katika Msikiti Mkuu wa Qum Iran, huku kikihudhuriwa na makundi mbalimbali ya wananchi.
Mwanzoni mwa kikao hicho, Ayatullah Jawadi Amuli, huku akiwapongeza wananchi kwa mnasaba wa kumbukumbu ya tarehe 13 Aban na kuenzi kumbukumbu ya mashahidi wa siku hiyo, alirejelea matukio ya kihistoria yanayohusiana na siku hiyo. Pia aliwaombea dua mashahidi wa Mapinduzi ya Kiislamu, hususan mashahidi wa tarehe 13 Aban pamoja na mashahidi wa hivi karibuni, akimuomba Mwenyezi Mungu Mtukufu awajaalie wawe pamoja na mashahidi wa Karbala.
Katika kikao hicho, akirejelea maneno yenye nuru ya Amirul-Muuminina Imam Ali (a.s.) kuhusu sifa za Mawalii wa Mwenyezi Mungu, alisema: Mawalii wa Mwenyezi Mungu ni watu ambao wao wenyewe wanaifanya Qur’ani kuwa msingi na mhimili wa maisha yao, na pia wanaifanya jamii kuwa yenye kufuata na kuongozwa na Qur’ani.
Akifafanua kwamba jukumu kuu la wanazuoni wa Hawza na vyuo vikuu ni kusimama pamoja na Qur’ani na kuyafanya maarifa ya wahyi kuwa msingi katika elimu na matendo, alisema: Amirul-Muuminina Imam Ali (a.s.) anasema kuhusu Mawalii wa Mwenyezi Mungu:
«بِهِمْ عُلِمَ الْكِتَابُ وَ بِهِ عَلِمُوا، وَ بِهِمْ قَامَ الْكِتَابُ وَ بِهِ قَامُوا»
Yaani, kwa baraka za Mawalii hao wa Mwenyezi Mungu, Kitabu cha Qur’ani kinafahamika na kueleweka, na kupitia kwao Qur’ani inasimamishwa na kutekelezwa katika jamii.
Hawza na vyuo vikuu vinawajibika kuifanya Qur’ani kuwa mhimili wa jamii
Ayatullah Jawadi Amuli, akisisitiza kwamba Qur’ani inapaswa kuwa mhimili wa elimu na harakati za jamii, alisema: Ikiwa tunataka Qur’ani iwe mhimili wa elimu katika jamii, basi Hawza na vyuo vikuu vinawajibika katika jambo hilo. Na ikiwa tunataka Qur’ani iwe mhimili wa kusimama na harakati za jamii, basi tena Hawza na vyuo vikuu vina wajibu huo. Ingawa sisi sote tuna wajibu, lakini jukumu la msingi katika eneo hili liko mabegani mwa wasomi, wanazuoni wa Hawza na vyuo vikuu.
Akigusia kwamba elimu ya Kitabu cha Mwenyezi Mungu hutimia kupitia wanazuoni na jamii ya wasomi, aliongeza: Mawalii wa Mwenyezi Mungu ni wale ambao Qur’ani ndiyo mhimili wa elimu yao, na Qur’ani pia huenea katika jamii kupitia kwao. Uwepo wa Qur’ani katika jamii, kuielewa Qur’ani na kuifanyia kazi kunapaswa kutekelezwa kupitia wanazuoni na wasomi wa Hawza na vyuo vikuu. Aidha, wanazuoni hao wenyewe wanapaswa kufanya harakati zao kwa kuongozwa na Qur’ani.
Ayatullah Jawadi Amuli, akisisitiza kwamba Qur’ani si kitabu cha kusomwa tu kwa ajili ya kupata thawabu, alisema: Qur’ani Tukufu ni kitabu cha utafiti wa kisayansi, kitabu hiki kinatufundisha namna ulimwengu ulivyo, ni nani aliyeuumba na mfumo wa ulimwengu umesimama juu ya misingi gani. Kila chembe katika ulimwengu huu imeumbwa kwa kuzingatia elimu, hesabu na mpangilio maalumu. Hakuna kitu chochote katika mfumo huu kilichopo bila sababu au bila kufuata utaratibu wa kielimu.
Akieleza kwamba mwanadamu hupata elimu zake kutokana na ulimwengu na mfumo wa uumbaji, alisema: Mhandisi wa kilimo anafahamu kwamba ili bustani iweze kutoa matunda, ni lazima kuwe na udongo unaofaa, mbegu zinazofaa, maji yanayofaa na mazingira mengine yanayohitajika. Ikiwa mambo hayo hayatapatikana, basi hakuna matunda yatakayopatikana, kila mti una mazingira na mfumo wake maalumu.
Elimu zote za mwanadamu zinatokana na ulimwengu huu na mfumo huu ambao Mwenyezi Mungu Mtukufu amemuwekea mwanadamu. Mwanadamu hakuwa na wala hana elimu yoyote aliyoipata kutoka kwake mwenyewe, bali elimu zote anazipata kutoka katika ulimwengu, kwa hiyo ulimwengu ni Kitabu cha Mwenyezi Mungu.
Katika kuendelea na maelezo yake, alisisitiza umuhimu wa wanazuoni na jamii ya wasomi kuwa na mazoea ya karibu zaidi na Qur’ani Tukufu, akisema: Haipaswi kuwa kwamba tunaisoma Qur’ani kwa ajili ya kupata thawabu za usiku wa Ijumaa pekee, ni wajibu wa kila mmoja wetu kuwa na ratiba maalumu ya Qur’ani.
Pendekezo langu ni kwamba, kama ambavyo tunakuwa na vipindi vya kawaida vya masomo, kila mmoja wetu awe na mpango wa kujifunza na kujadili Qur’ani nzima. Si lazima tuanze moja kwa moja na tafsiri za kina, bali tunapaswa kuelewa maudhui na ujumbe mkuu wa aya na kufahamu Qur’ani inataka kutuambia nini, na pale itakapohitajika kupata ufahamu zaidi, tunaweza kurejelea vitabu vya tafsiri.
Ayatullah Jawadi Amuli, akiendelea na maelezo yake na kurejelea juhudi za kielimu za vizazi kadhaa vya watafiti katika kuandaa kitabu cha tafsiri ya Qur’ani kinachoitwa Tafsir Tasnim, alisema: Kazi hii ni matokeo ya juhudi za Hawza, si kazi binafsi ya mtu mmoja, bali ni matokeo ya takribani miaka 40 ya juhudi na jitihada za vizazi vinne vya kielimu ndani ya Hawza. Kila kizazi kilitumia takribani miaka kumi kikifanya kazi katika njia hii kwa kutumia fikra, mitazamo na uelewa wake wa kielimu wa Hawza na vyuo vikuu. Katika mchakato huo, maswali yaliibuliwa na majibu yake yakatolewa.
Pamoja na juhudi zote hizo, yale yaliyoandikwa bado ni tone moja tu katika bahari ya Qur’ani Tukufu. Hata hivyo, jambo muhimu ni kwamba sisi sote tunapaswa kuwa wasomaji na watafiti wa Qur’ani.
Ushindi wa haki dhidi ya batili ni ahadi ya hakika ya Qur’ani Tukufu
Katika sehemu nyingine ya hotuba yake, Ayatullah Jawadi Amuli, akizungumzia Sunna ya Mwenyezi Mungu katika mapambano kati ya haki na batili, alisema: Qur’ani Tukufu, katika matukio yote ya zamani na ya sasa, kila inapozungumzia mapambano kati ya haki na batili, inatufundisha kwamba haki ndiyo yenye ushindi, haiwezekani batili isimame na kupambana dhidi ya haki kisha hatimaye ikashinda.
Mwenyezi Mungu anasema:
﴿لِیُحِقَّ الْحَقَّ وَیُبْطِلَ الْبَاطِلَ﴾
“Ili Aithibitishe haki na kuibatilisha batili.”
Hii ni kanuni ya jumla na hukumu ya msingi ya mfumo wa uumbaji.
Ayatullah Al-Udhma Jawadi Amuli, akigusia mashambulizi ya maadui na kuuawa kishahidi Kiongozi Mkuu, wasomi, pamoja na kundi la wananchi na wanajeshi wa kujitolea wa Basij, hususan watoto wa Minab, alisema: Ingawa maadui wa kigeni wamefanya mashambulizi, kusababisha hasara na kuwaua kishahidi wapendwa wetu, lakini hatupaswi kusahau ahadi ya Mwenyezi Mungu, kushindwa Marekani na Israel ni jambo la yakini.
Qur’ani inawaambia watu wa haki wasiwe na wasiwasi. Katika kila mahali ambapo kuna vita kati ya haki na batili, haki ndiyo itakayoshinda, hili si jambo la kutabiri habari za ghaibu pekee, bali ni taarifa kuhusu Sunna na mfumo ambao Dhati Tukufu ya Mwenyezi Mungu ameuweka katika ulimwengu huu.
Ayatullah Jawadi Amuli alisisitiza: Qur’ani inasisitiza kueleza masuala haya ili jamii ya waumini ifahamu kwamba katika mapambano kati ya haki na batili haipaswi kuingiwa na hofu wala kusitasita, ushindi wa haki ni ahadi ya hakika ya Mwenyezi Mungu, na kufanikiwa Uislamu na Waislamu ni jambo la yakini.
Uislamu ni dini inayojenga watu wenye moyo wa kishujaa na ushujaa
Katika kuendelea na hotuba yake, akirejelea riwaya zinazohusiana na kuilinda nchi na kukabiliana na wavamizi, alisema: Miongoni mwa maagizo rasmi ya Uislamu ni kulea watu wenye moyo wa kishujaa, wapambanaji na wenye ujasiri, Uislamu ni dini inayolenga kuwalea wanadamu wawe watu jasiri na wenye moyo wa kishujaa.
Ayatullah Jawadi Amuli, akirejelea riwaya kutoka kwa Imam Muhammad Baqir (a.s.) na Imam Jaafar Swadiq (a.s.) kuhusu mwenendo na misimamo ya Amirul-Muuminina Imam Ali (a.s.) katika kuilinda nchi na kukabiliana na wavamizi, alisema: Riwaya hizi hazizungumzii hukumu za Swala wala masuala ya kawaida ya maisha. Bali ndani yake yamenukuliwa maneno kutoka kwa Amirul-Muuminina Imam Ali (a.s.) na babu yake mtukufu, yanayoeleza kwamba mtu anapaswa kusimama imara dhidi ya mvamizi anayeshambulia ardhi na nchi yake.
Wanasema: Hawa wapiganaji wanaofanya vita na kuvamia ardhi yenu, yaani Marekani na Israel ambao wameivamia nchi yenu, wauweni; nami ninachukua dhamana ya damu yao!
Ayatullah Jawadi Amuli, akifafanua umuhimu wa kuwa macho katika medani ya ulinzi, alisema: Amirul-Muuminina Imam Ali (a.s.), katika mojawapo ya barua zake alizowaandikia wapiganaji, anasema:
«وَ لَا تَذُوقُوا النَّوْمَ إِلَّا غِرَاراً أَوْ مَضْمَضَةً»
“Msionje usingizi isipokuwa kwa muda mfupi sana au kwa kiwango cha lazima.”
Hii ni sawa na mtu aliyefunga anapoweka maji kinywani mwake kwa ajili ya kusukutua, lakini anakuwa mwangalifu asiyameze. Vivyo hivyo, mpiganaji anapokuwa katika jukumu la kulinda na kusimamia eneo lake la ulinzi, anapaswa kujiepusha na usingizi wa kughafilika na kuendelea kuwa macho na makini wakati wote.
Akisisitiza kwamba jukumu hili halihusu wanajeshi na viongozi wa serikali pekee, alisema: Sisi sote tuna wajibu, na kila mmoja wetu ana jukumu lake, katika kuulinda mfumo huu sote tunawajibika katika masuala ya maadili ya jamii, uchumi, kukidhi mahitaji ya wananchi na kuwaandalia wafanyakazi fursa za ajira, katika mambo haya yote, kila mmoja wetu ana wajibu wake.
Ayatullah Jawadi Amuli, akieleza matumaini yake kuhusu kuendelea heshima na nguvu ya mfumo wa Kiislamu, alisema: Tunatumai kwamba mfumo huu, kwa baraka za Qur’ani na Ahlul-Bayt (a.s.), utakabidhiwa kwa namna njema kwa uwepo mtukufu wa Walii wa Zama, Imam Mahdi (a.j.f.), na kwamba uadui wa maadui nao utaishia katika udhalili na kushindwa.
Mwisho wa hotuba yake, aliomba dua kwa ajili ya heshima na utukufu wa jamii na washiriki wa kikao hicho. Alimuomba Mwenyezi Mungu Mtukufu awajalie wote heshima, utukufu na adhama ya Qur’ani, na awajaalie mashahidi wa Mapinduzi ya Kiislamu na mashahidi wa kuutetea Uislamu wawe pamoja na mashahidi wa Karbala.
Maoni yako